Shirika la Habari la Hawza - Miongoni mwa mambo yanayopendwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni toba; kwa hivyo Imam Sajjad (a.s.) anamwomba Mwenyezi Mungu kwa maneno haya:
“اللَّهُمَّ ... صَیِّرْنَا إِلَی مَحْبُوبِکَ مِنَ التَّوْبَةِ.”
“Ee Mwenyezi Mungu! Tuongoze kwenye njia ya toba inayokupendeza Wewe.” (2)
Sherehe:
Toba ni dhihirisho la fadhila na rehema isiyo na mipaka ya Mwenyezi Mungu.
Toba inamaanisha kwamba Mwenyezi Mungu kamwe haridhii kuachana na mja Wake; kwa hivyo njia ya kurejea kwa Mwenyezi Mungu ipo wazi kwa mja katika kila wakati na kila mahali.
Katika hadithi ya kuvutia sana, Imam Baqir (a.s.) kuhusu ubora wa toba amesema:
“Mwenyezi Mungu Mtukufu hufurahi zaidi kwa toba ya mja Wake kuliko mtu aliyepoteza mnyama wake wa kupanda, na azma yake katika usiku wa giza katika jangwa, kisha ghafla akavipata tena.” (2)
Jambo la kuzingatia zaidi ni kwamba uwezo wa kutubu na kurejea kwa Mwenyezi Mungu wenyewe unatoka kwa Mwenyezi Mungu!
Qur’ani Tukufu inasema:
“ثُمَّ تَابَ عَلَیْهِمْ لِیَتُوبُوا إِنَّ اللَّهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِیمُ.”“Kisha Mwenyezi Mungu akawafikia kwa rehema Yake, (na akawapa tawfiki) ili watubu; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba na Mwenye rehema.”
Kwa hakika, toba ya mwanadamu imo kati ya toba mbili za Mwenyezi Mungu: kwanza, Mwenyezi Mungu humpa mja wake uwezo wa kutambua udhaifu na kumrejea, kisha mja hutubu, na hatimaye Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa rehema Zake huikubali toba yake.
Hakika Mungu huyu anastahili kusifiwa.
Lakini jambo linalofanya uhusiano wa mja na Mola wake uwe wa ajabu zaidi katika “kurejea huku” ni hatua ambazo Mwenyezi Mungu huzichukua kwa ajili ya mwenye kutubu.
Hatua ya kwanza ya Mwenyezi Mungu kwa mja anaetubia ni kwamba hukubali toba yake.
“هُوَ الَّذِی یَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبادِهِ.”
“Yeye ndiye anayekubali toba kutoka kwa waja Wake. (4)
Hatua ya pili, Mwenyezi Mungu humsamehe dhambi na maovu yake.
“وَ یَعْفُوا عَنِ السَّیِّئاتِ.”
“Na husamehe maovu.” (5)
Hatua ya tatu, Mwenyezi Mungu hubadilisha dhambi na maovu ya mja wake kuwa mema na mazuri.
“فَأُوْلئِکَ یُبَدِّلُ اللَّهُ سَیِّئاتِهِمْ حَسَناتٍ.”
“Hao Mwenyezi Mungu atazibadilisha dhambi zao kuwa mema.” (6)
Na hatua ya mwisho ya Mwenyezi Mungu ndio yenye kupendeza zaidi: Mwenyezi Mungu humwambia mwenye kutubu, ‘Nakupenda.’
“إِنَّ اللَّهَ یُحِبُّ التَّوَّابِینَ.”“Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaotubu.” (7)
Rejea:
1. Sahifa Sajjadiyya, Dua ya Tisa.
2. Bihar al-Anwar, Juzuu ya 6, uk. 90.
3. Surat Tawba, aya ya 118.
4. Surat Shura, aya ya 25.
5. Aya hiyo hiyo.
6. Surat Furqan, aya ya 70.
7. Surat Baqarah, aya ya 222.
Imeandaliwa na Idara ya Elimu na Utamaduni ya Shirika la Habari la Hawza,
Maoni yako